Kwa mara nyingine tena mwenyekiti wa shirika la uchapishaji vitabu la Jomo Kenyatta Walter Nyambati amejitokeza kutangaza wazi nia yake ya kugombea ugavana katika kaunti ya Nyamira. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye shule ya upili ya wavulana kule Nyambaria siku ya Jumapili, Nyambati alisema kuwa ana nia ya kugombea ugavana kwenye uchaguzi mkuu ujao katika kaunti ya Nyamira. 

"Ningependa kumwambia mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire asiwe na hofu kwamba tutakuwa tukibishana naye kwenye uchaguzi wa kiti cha ubunge kwa maana nina nia ya kuwania ugavana katika kaunti hii ili kuwafanyia wananchi kazi," alisema Nyambati. 

Nyambati aidha alimtaka waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba shule za upili za umma zinapokea vifaa vya kutosha kwenye maaabara. 

"Ikiwa kwamba waziri Matiang'i kwa sasa unashikilia wadhifa wa waziri wa elimu nchini ni ombi langu kwako kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba shule zetu za umma zimepokea vifaa vya kutosha kwenye maabara kwa sababu huenda ukapelekwa kuhudumu kwenye wizara nyingine kabla ya shule zetu kufaidi," aliongezea Nyambati.