Aliyekuwa mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba Walter Nyambati amewashtua wapiga kura wa eneo bunge hilo, baada yake kutishia kujitoa uhai iwapo mbunge wa sasa Timothy Bosire atamshinda kwenye uchaguzi mkuu ujao. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Nyambati aliyasema haya wakati alipokuwa akihutubu kwenye hafla ya maombi ya marehemu Sabina Abuya, ambaye ni mamake aliyekuwa mbunge wa zamani wa eneo hilo Abuya Abuya siku ya jumanne.

Nyambati aliongeza kusema kuwa ana hakika ya kuibuka na ushindi kwenye kinyanganyiro hicho cha ubunge, huku akisema kuwa rekodi yake ya utendakazi ndiyo itakayompa ushindi. 

"Nina hakika kwamba nitaibuka na ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa rekodi yangu ya hapo awali itaniwezesha kumpiku mbunge wa sasa Timothy Bosire," alisema Nyambati. 

Mwenyekiti huyo wa shirika la uchapishaji vitabu la Jomo Kenyatta Foundation aliongeza kusema kuwa kamwe hatokubali matokeo ya tume ya uchaguzi iwapo hatotangazwa kuwa mshindi kwa kuwa jinsi mambo yalivyo, wapiga kura wa eneo hilo wamechoka na uongozi wa mbunge wa sasa na kuwa atajitoa uhai iwapo hilo halitatokea. 

"Nimetembea kote Kitutu Masaba na jinsi hisia za watu zilivyo ni bayana kwamba nitaibuka na ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao, na iwapo tume ya uchaguzi haitonitangaza mshindi basi sitayakubali matokeo hayo, iwapo Bosire atatangazwa mshindi nitachukua kamba na kujinyon'ga," alisema Nyambati. 

Mbunge huyo wa zamani aidha alimshutumu mbunge wa sasa kwa kujipigia upato wa kisiasa kupitia miradi aliyoianzisha alipokuwa mbunge.