Joka lililoingia darasani wakati masomo yakiendelea katika shule ya msingi ya Kareka, lilisimamisha masomo shuleni humo kwa siku nzima huku walimu na wanafunzi wakipambana kuliua.
Mwalimu mkuu shuleni humo, Velma Ogeto, amewaomba maafisa wa kulinda wanyama mwitu kuwahakikishia wananchi wanaoishi katika maeneo ya misitu usalama kwa kuwaondoa wanyama mwitu ambao hurandaranda ovyo mitaani na kuhatarisha maisha ya wakaazi.
Ogeto aliomba idara ya wanyama pori kushika doria vikamilifu viunga mwa mji huo ulioko Maseno, ili kumaliza visa vya wanyama hao kuwashambulia wananchi kwenye makazi yao.
Nyoka huyo alionekana chini ya dawadi la mwanafunzi mmoja kwenye darasa la nne, na kusababisha masomo kusimamishwa siku nzima.
“Nawaomba maafisa wa kulinda wanyama pori kuwakakikishai wananchi usalama wao kutokana na wanyama ambao ni hatari kwa maisha ya binadamu. Sasa ikiwa nyoka mkubwa kama yule angemuuma mwanafunzi saa hii tungekua labda tunaomboleza kifo au hata vifo,” alisema Ogeto.
Aidha naibu huyo wa mwalimu mkuu pia aliomba wakaazi wa eneo hilo kutunza mazingira yao kwa kuyaweka safi, ili kupunguza hatari ya kushambuliwa na wanyama pori na hata magonjwa yanayosababishwa na mazingira machafu.
Akihutubu kwenye mkutano na wazazi shuleni humo, Ogeto pia alianzisha kampeni ya kung’arisha mazingira ya eneo hilo kwa kufyeka misitu iliyo karibu na makazi pamoja na shule.