Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Kisumu imesutwa vikali kufuatia utepetevu katika idara ya kukabiliana na majanga hasaa ya moto unapozuka katika maeneo mbali mbali Kisumu.

Mbunge wa Kisumu ya Kati Ken Obura anasema ipo haja kwa serikali ya kaunti hiyo chini ya gavana Jack Ranguma kuzingatia umuhimu wa kuimarisha kikosi cha kukabiliana na mikasa na kuhakikisha kuwa vifaa vya kukabiliana na mikasa ya moto iko katika hali nzuri.

Obura amependekeza kitengo cha kukabiliana na mikasa kuongezewa mgao wa fedha ili kujiimarisha zaidi na kuwekwa katika maeneo mbali mbali ili kuimarisha utendakazi wake badala ya kuzingatiwa eneo moja pekee.

Kadhalika amesisitiza kuwekwa kwa tawi la idara ya kukabiliana na mikasa katika eneo la Kibuye ili kudsaidia kukabiliana na mikasa ya moto ambayo imekuwa ikishuhudiwa katika soko hilo, mkasa wa tatu wa moto ukishuhudiwa usiku wa kuamkia Jumamosi ambapo mali ya mamilioni ya pesa ya wakaazi ilipata kuteketea.

"Ilibidi halmashauri ya ndege -Kenya airport Authority, kusaidia katika juhudi za kukabiliana na moto uliotokea katika soko la Kibuye, hali inayoonyesha unyonge katika idara ya mikasa Kisumu,’’ alidokeza Obura.