Seneta wa Kaunti ya Kisii Chris Obure, ameitaka idara ya kushughulikia masuala ya moto katika kaunti hiyo kuhakikisha kuwa magari ya zimamoto yana maji ya kutosha ili kukabiliana na visa vya dharura.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumapili katika mji wa Kisii, seneta huyo, alisema kuwa kuna haja ya magari ya idara hiyo kuwa na mahitaji yote na kufanyiwa huduma za kiufundi kila mara, ili kunapotokea mikasa ya moto, iwe tayari kukabili mikasa hiyo.
Aliiomba serikali ya kaunti kufanya uchunguzi na kutoa ripoti ya chanzo cha moto ambao uliteketeza mali ya wafanyibiashara siku ya Ijumaa karibu na kituo cha mafuta cha Falcon.
“Idara ya zimamoto inahitajika kuwa tayari wakati wowote kunapotokea dharura, hasa ikizingatiwa kuwa kaunti yetu imeshuhudia visa vingi vya moto. Naomba pia uchunguzi ufanywe kwa haraka ili kubaini chanzo cha moto huo, ili wale walioathirika wapate ukweli na kuweza kuendelea na biashara zao,” alisema Obure.
Kufikia sasa, hakuna ripoti yoyote imetolewa na idara ya polisi kuhusiana na moto huo, huku wenye biashara karibu na eneo hilo wakisema kuwa huenda moto huo ulisababishwa na hitilafu ya nguvu za umeme.
Moto huo ulizuka usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa katika nyumba za biashara zilizoko kwenye barabara ya kutoka mjini Kisii kuenda soko kuu la Daraja Mbili.