Seneta wa kaunti ya Kisii Chris Obure amewaunga viongozi wa tume ya walimu nchini Knut kuendelea kufanya mgomo hadi serikali iwape hela za nyongeza za mshahara wao kati ya asilimia 50 na 60 ilivyoamuru mahakama kuu.
Obure, ambaye alikuwa akiongea mjini Kisii siku ya Jumapili, aliwashtumu baadhi ya viongozi wa kutoka serika kuu, ambao wamekuwa wakiingiza siasa kwenye suala hilo la walimu, na kumtaka rais Uhuru Kenyatta kulipa suala hilo mwongozi na kuacha kufuata ushauri wa wanasiasa kutoka mlengo wa JAP ambao wanajitakia makuu.
Kiongozi huyo alilalamikia njia ambayo serikali ya Jubilee inachukulia suala hilo, huku akisema wanaoumia ni watoto wa maskini ambao wanasomea shule za umma, huku wale wanaosomea shule za kibinafsi, ambazo hujumuisha watoto wa wanasiasa, wanaendelea kufaidi.
Aliwataka rais na naibu wake kukaa na kutafuta suluhu, ikizingatiwa kuwa wanafunzi wa kidato cha nne na wale wa darasa la nane wanaelekea kufanya mtihani wao wa kitaifa, na huenda wakaathirika kutokana na kukosa kufunzwa.
Pia aliwataka waziri wa elimu Jacob Kaimenyi pamoja na mkurugenzi mkuu wa tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC Dkt Lydia Nzomo kuacha kuwatishia walimu, akisema kila mkenya ana haki ya kutetea msimamo wake inavyosema katiba ya nchi.
Wito huu umetolewa huku mgomo huo ukiingia wiki ya pili hii leo, Jumatatu, ambapo tume ya TSC imeonya walimu ambao watasusia kurudi watasimamishwa kazi na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kushiriki kwenye mgomo kinyume cha sheria.