Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima amesema kuwa hajuti kukigura chama cha ODM.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Likoni, Mwahima alisema kuwa alikihama chama hicho baada ya kugundua kuwa kimekosa ajenda.

Mbunge huyo alisema ana imani kuwa atasalia madarakani kupitia chama cha Jubilee.

“Nilikigura chama cha ODM baada ya kugundua kuwa hakina ajenda. Mimi siwezani na mambo ya vurugu. Umri wangu hauniruhusu kushiriki maandamano,” alisema Mwahima.

Aidha, alisema kuwa watu wanaojaribu kumharibia jina hawatafaulu kwa sababu anafurahia uungwaji mkono kutoka kwa wakaazi wa Likoni.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko amewasuta wanasiasa walioasi chama cha ODM.

Akizungumza katika eneo la Likoni alipotangaza rasmi nia yake ya kuwania kiti cha ubunge cha eneo hilo, Mboko aliwakosoa wabunge hao kwa kukihama chama kilichowapeleka bungeni.

Aidha, aliwakejeli wanasiasa waliohamia chama cha Jubilee, kwa kudai kuwa walichukua hatua hiyo baada ya kushuritishwa.

Mwakilishi huyo alisema kuwa bado chama cha ODM kinajivunia  umaarufu mwingi.

“Mwaka wa 2017 nitawania kiti cha ubunge kupitia tiketi ya ODM na nina imani kuwa nitaibuka mshindi,” alisema Mboko.

Aidha, Mboko aliukosoa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, na kumkashifu kwa kuagiza wakaazi wa shamba la Waitiki kulipa ada ya ardhi hiyo.

“Iwapo Rais Kenyatta anataka wakaazi wa Pwani wamuunge mkono, sharti awafanyie maendeleo,” alisema Mboko.