Mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba Walter Nyambati amesema kuwa chama cha ODM katika Kaunti ya Nyamira ni kama mbwa anayebweka bila kung'ata.
Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano wa maombi katika uga wa Afraha, Nyambati alisema kuwa chama cha ODM kimepoteza umaarufu wake katika Kaunti ya Nyamira, na kumtaja Gavana wa Nyamira John Nyagarama kama kiongozi anayedhihirisha tabia halisi ya viongozi wa ODM.
"Nyagarama, Rasanga, Ojamong na Hassan Joho ndio viongozi waliotuonesha Cord ni nini. Hawa ndio viongozi wanaosema bila kutenda.Wanamnyoshea rais kidole cha lawama kila wakati ilhali wameshindwa kuhudumia kaunti zao,” alisema Nyambati.
Nyambati aidha aliwataka wakaazi wa Nyamira kupiga kura kwa busara wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, huku akiongeza kuwa serikali ya Jubilee itashinda uchaguzi huo kwa ushindi wa kishindo.
"Tunasubiri mwaka 2017 ili tuwaoneshe kuwa wao ni mbwa wanaobweka bila kung'ata. Tutashinda uchaguzi huo kwa kishindo kutoka viti vya wawakilishi wadi hadi kwa kiti cha urais," alisema Nyambati.
Nyambati aliwataka wakaazi kutopotoshwa kwa kupewa pesa na ahadi za miradi ya uwongo.
Mbunge huyo wa zamani pia alitoa wito kwa Nyagarama kutatua mzozo wa mpaka unaokumba Kaunti za Nyamira na Kisii.