Chama cha ODM kimeeleza kughadhabishwa na hatua ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC, kutupilia mbali sahihi za kampeni ya Okoa Kenya kwa madai kuwa haikufikisha idadi inayohitajika kisheria.
Katika mahojiano na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa ODM tawi la Mombasa, Mohammed Hatimy, aliilaumu IEBC kwa kutochapisha majina ya watu walioandikisha sahihi yao kufanikisha zoezi hilo.
Hatimy alidai kuwa Cord ilikusanya sahihi ya watu zaidi ya milioni moja, tofauti na idadi ya laki nane iliyoripotiwa na IEBC siku ya Jumanne baada ya kuzikagua sahihi hizo.
“Kama Cord tulipata zaidi ya sahihi milioni moja kutoka kwa wananchi wanaotaka katiba ifanyiwe mageuzi. Tulishangaa tulipoambiwa hatukufikisha idadi inayotakikana,” alisema Hatimy.
Aidha, Hatimy alidai kuwa uamuzi wa IEBC ulichochewa kisiasa na kudokeza kuwa Cord itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kuwa kura ya maoni inaandaliwa.
Siku ya Jumanne, Tume Huru ya uchaguzi na Mipaka IEBC ilitupilia mbali sahihi za kampeni ya Okoa Kenya zilizowasilishwa na mrengo wa Cord kwa kile ilikitaja kama kutoafikia idadi inayohitajika kwa mujibu wa sheria.