Mbunge wa eneo bunge la Bomachoge Chache Kaunti ya Kisii, amesema hazina ya ustawi maeneo bunge haitaondolewa kamwe, ila itasalia kuwa katika bunge la kitaifa na kuendelea kutoa usaidizi kwa wananchi wa Kenya kwa kufanya maendeleo kikamilifu.
Hii ni baada ya kusemekana kuwa hazina hiyo ya CDF haitakiwi kuendelea jambo ambalo mbunge Simon Ogari alisema halitakuwa kamwe kwani hazina hiyo imeleta maendeleo mengi zaidi kwa wananchi wote hasa katika sehemu za mashinani.
Kulingana na mbunge huyo, kamati ya bunge inayosimamia hazina hiyo ya CDF katika bunge la Kitaifa ilitembea kote nchini kutafuta maoni ya wananchi ikiwa watahitaji iondolewe au isalie kuwa katika bunge la Kitaifa.
Alisema maoni mengi ya wananchi yalipendekeza hazina hiyo kuendelea jambo ambalo mbunge alisema halitageuzwa na mahakama ila hazina hiyo iendelee milele.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Tendere, alipokuwa anatoa pesa hizo za hazina ya CDF kwa miradi mbalimbali ya maendeleo, mbunge huyo alisema hazina ya CDF itaendelea kwani ikiondolewa maendeleo hayatafanyika mashinani.
Mbunge huyo alitembea eneo la Mesese, Sengera na Tendere na akatoa shillingi million 30 ili zifanye kazi za maendeleo katika bunge hilo.
Baadhi ya miradi ambayo ilipokezwa pesa hizi ni kati ya mradi wa maji ambao ulikabidhiwa shilling million 4.4, mradi wa hospitali ulipokezwa million 4, vituo vya kupima majani chai vilipatiwa million 1.2, na shule za upili zikakabidiwa millioni 11.5.
“Hazina ya CDF itaendelea chini ya bunge la Kitaifa ili kusaidia na kuleta maendeleo katika sehemu zote za mashinani,” alisema Ogari.