Mbunge wa zamani wa eneo bunge la Kitutu Masaba Mwancha Okioma amejitokeza kumtaka Rais Uhuru Kenyatta kuacha kushirikiana kisiasa na naibu Rais William Ruto iwapo ana nia ya kuchaguliwa tena.
Akihutubu kwenye mkutano wa hadhara kule Gesima siku ya Jumatatu, Okioma alisema kuwa umaarufu wa naibu rais William Ruto unaendelea kudidimia miongoni mwa wananchi,huku akiongezea kuwa asilimia kubwa ya wakenya wanaendelea kupoteza imani kwa serikali ya Jubilee.
“Kwa kweli hii serikali ya Jubilee ni miongoni mwa serikali fisadi zaidi kuwahi kuongoza taifa hili, ikizingatiwa na madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka yanayomkumba naibu rais William Ruto,” alisema Okioma.
Akizungumzia sakata ya ufujaji wa mamillioni ya pesa kutoka kwa shirika la kitaifa la vijana NYS ambapo wanachama wa chama cha URP wametajwa na aliyekuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru, Okioma alisema yafaa Ruto achukue hatua ya kuwaamrisha waliotajwa kujiuzulu ili kuruhusu uchunguzi kufanyika.
“Hivi maajuzi mlisikia baadhi ya wanasiasa wa URP ambao ni washirika wa karibu wa naibu Rais William Ruto hasa seneta kipchumba Murkomen, mbunge Aden Duale na Farook Kibet wakiwa miongoni mwa washukiwa wakuu waliotajwa, na ndio sababu hasa namtaka Rais Uhuru kumtenga Ruto iwapo hataki kujihuzisha na viongozi wafisadi,” alisema Okioma.
Okioma aidha alisema kuwa huenda naibu rais William Ruto ameanza kupoteza umaarufu wa kisiasa katika mkoa wa Bonde la Ufa, ikizingatiwa kwamba baadhi ya wanasiasa wa chama cha URP wanaendelea kupinga mbinu zake za uongozi.