Wakili wa masuala ya kisheria Okongo Omogeni amejitokeza kushtumu vikali kisa ambapo wadumisha usalama wawili vijijini kule Bokeira katika eneo la wilaya ya Nyamira kaskazini waliuliwa kwa kupigwa risasi na washukiwa wa ujambazi wiki mbili zilizopita.
Akihutubu kwenye hafla ya mazishi ya mmoja wa wadumisha usalama hao Paul Nyanumba, alisema kuwa hatia kwa wadumisha usalama wanaostahili kudumisha usalama vijijini kuuliwa bila makosa.
"Inakuwaje kwamba watu wanaodumisha usalama vijijini wanaweza kuuliwa na magaidi na kwa kweli hiki ni kitendo cha unyama ambacho kinastahili kushtumiwa vikali," alisema Omogeni.
Omogeni aidha aliongeza kwakuitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kuwachukulia hatua kali wale watakaopatikana kuhusika na mauaji hayo.
"Tunafahamu kuwa tayari washukiwa zaidi ya kumi wametiwa mbaroni huku wengine wakiachiliwa kwa dhamana ila ninaloiomba serikali kufanya nikuhakikisha kwamba uchunguzi wa kina umefanywa ili watakaopatikana kuhusika na mauaji haya kuchukuliwa hatua kali za kisheria," aliongezea Omogeni.