Wanaofanya kazi chini ya mkataba wa kandarasi na wanafunzi wanaopokea mafunzo katika hospitali ya Nyamira Level Five sasa wana kila sababu ya kutabasamu.
Haya yanajiri baada ya Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o kuiomba Serikali ya kaunti hiyo kuwapa fursa ya kwanzakatika zoezi ya kuajiri madaktari wapya.
Akiongea siku ya Jumapili katika mji wa Nyamira, seneta huyo alisema kuwa watu hao wamekuwa wakivumilia kwa wakati mrefu kufanya kazi bila kuajiriwa na serikali na kusema ni vyema wafurahie matunda yao ya uvumilivu kuhudumu katika hospitali hiyo.
"Wale wamekuwa wakihudumu katika hospitali ya Nyamira Level Five kama wahudumu wa kandarasi wakumbukwe kwanza halafu wengine wapate fursa ya pili maana hao ndio wanajua jinsi kazi imekuwa ikifanyika katika hospitali hiyo tangu waingie huko," alisema seneta Okong’o.
"Naiomba bodi ya kuajiri watu katika serikali hii ya Nyamira kuonyeshe uwazi kwa kuwapa fursa ya kwanza wale wapo chini ya kandarasi na wanafunzi kufanya kazi ya kutibu wagonjwa," aliongeza Okong’o.
Wakazi wa kaunti hiyo walifurahishwa na ombi la seneta huyo huku wengi wakisema kuwa mapendekezo haya ndio yatakuwa njia ya haki na uwazi kwa wakazi wote wa kaunti hiyo ya Nyamira haswa watu wanapoajiriwa.
"Bodi hiyo ya kuajiri wafanyikazi ikifanya hivyo kwa kuwaajiri wanafunzi wale wamekuwa wakihudumia wagonjwa na wale walio chini ya mkataba wa kandarasi hatutakuwa na lolote la kupinga maanake itakuwa tayari imeonyesha haki kwa mkazi wa kaunti hii," alisema Kevin Mochama mkazi wa Nyamira.