Mbunge wa Kibera, Ken Okoth amemsuta Rais Uhuru Kenyatta kufuatia matamshi yake kwamba hakuna Mkenya yeyote atayehukumiwa katika mhakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC.
Okoth alimkumbusha Rais Kenyatta kwamba taifa la Kenya lina jukumu la kuheshimu mikataba ya kimataifa ikiwemo mkataba wa Roma uliobuni ICC.
“Rais akikosea na tumkosoe. Aanafaa kuelewa wala si kuchochea wananchi kwa kusema mambo ambayo si ya kisheria,” alisema Okoth.
Mbunge huyo aliongeza kuwa mahakama hiyo yenye makao yake mjini, The Hague, Uholanzi, ni muhimu katika kupambana na hulka ya watu kufanya makosa bila kuheshimu sheria na kuutaka uongozi wa Jubilee kufuata taratibu zilizopo iwapo unataka kujiondoa katika mkataba huo wa Roma.
“Hizi ni baadhi ya sheria za Kenya na sisi kama wakenya tunafaa kuzizingatia ikiwemo sheria ya ICC ya mkataba wa Roma na kwa hivyo, kama Rais Kenyatta hataki, itawalazimu kama Jubilee kujiondoa wenyewe kwa mkataba huo. Kwa sasa bado tuko kwenye ICC na inaweza kutumika kuondoa mambo ya ukandamizaji,” aliongeza Okoth.