Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA jimbo la Nakuru, Abdul Noor amemsuta katibu mkuu wa chama hicho Onyango Oloo kwa kutangaza kuwa chama hicho kitaitisha maandamano ya kitaifa ya kuunga mkono tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC).

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Noor alisema  ni makosa kwa Oloo kuitisha maandamano wakati chama cha TNA kimekuwa kikipinga maandamano ya CORD.

Akizungumza Jumanee mjini Nakuru, Noor alisema itakuwa kosa kubwa sana iwapo chama cha TNA kitaitisha maandamano na kusema kuwa hilo huenda likazua vurugu kati ya wafuasi wa CORD na Jubilee.

"Nimemsikia Onyango Oloo akisema kuwa ataitisha maandamano ya wafuasi wa jubilee kote nchini na nataka kumuambia kuwa awache kuwapotosha wafuasi wa TNA ," alisema Noor. "Huwezi kuzima moto kwa kuwasha moto mwingine na Oloo anafaa kuelewa hilo. Iwapo TNA wataitisha maandamano basi taifa huenda likatumbukia katika machafuko,"aliongeza.

Oloo alitangaza kuwa chama cha TNA kitaitisha maandamano ya kitaifa iwapo muungano wa CORD utaendelea kuandaa maandamano ya kuwataka makamishina wa IEBC kuondoka afisini.