Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwakilishi wa wadi ya Bogichora Beauttah Omanga ameonyesha kutoridhishwa kwake na jinsi serikali kuu imewaondoa watoto 198 mayatima na wasiojiweza katika jamii kutoka kwa orodha ya wale wanaopokea msaada wa shilingi elfu mbili kila mwezi kwa madai kuwa wamefikisha umri wa miaka 18.

Akiongea siku ya Jumanne katika wadi hiyo kwenye mkutano wa wazazi na walezi wa watoto hao, Omanga alisema kuwa baadhi ya watoto ambao wameondolewa kwenye orodha hiyo hawajafikisha miaka 18, na kuongezea kuwa haelewi sababu ya kuondolewa kwa watoto wengi kutoka wadi hiyo.

"Watoto wengi ambao wameondolewa kutoka kwa mpango huo wa serikali kuu wa kupata shilingi elfu Sh2,000 kila mwezi wako na umri mdogo wa miaka kuanzia 8 hadi 10, na hayo ni makosa kwa sababu watoto hao hawana pa kuenda," alisema Omanga.

Omanga amesema kuwa hata baada ya kufika kwenye afisi ya watoto kwenye kaunti hiyo hajapata jibu la kuridhisha, kwani maafisa husika hawajampa suluhisho la kudumu.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa maswala ya watoto katika kaunti ya Nyamira Samuel Masese amekanusha madai hayo na kusema kuwa hamna mtoto hata mmoja ameondolewa kwenye orodha hiyo.

"Nakubali kuwa mtoto akifikisha umri wa miaka 18 anaondolewa kwa orodha, lakini kwa hivi sasa hatujaondoa yeyote kwa sababu tunasubiri mawasiliano kutoka kwa serikali kuu," alisema Masese.

"Yeyote ambaye ana maswali ataweza tutembelea kwa ofisi zetu mjini Nyamira ili ajue ukweli wa mambo," aliongezea Masese.