Mwakilishi wa eneo wodi ya Bogichora Beautah Omanga ameshtumu vikali hatua ya naibu Rais William Ruto kuitaka jamii nzima ya Abagusii kujiunga na muungano wa Jubilee.
Kwenye mahojiano ya simu siku ya Jumatatu, Omanga alisema kuwa Ruto hastahili kuishinikiza jamii ya Abagusii kujiunga na muungano wa Jubilee.
"Haya matamshi ya naibu rais kuitaka jamii ya Abagusii kujiunga na muungano wa JAP kabla ya uchaguzi mkuu ujao hayastahili kamwe kwa maana serikali hii imewafeli pakubwa wakenya," alisema Omanga.
Omanga aidha alimtaka Ruto kuwaeleza bayana wakenya miradi ya maendeleo ambayo serikali ya Jubilee imeafikia tangu ilipoingia mamlakani.
"Visa vya ufisadi vinaendelea kukithiri serikalini, na badala Ruto atueleze mipango serikali ya Jubilee inayo ili kukabili ufisadi ni ipi na hata kuwaeleza wakenya miradi ya maendeleo ambayo serikali imeafikia tangu iingie mamlakani," aliongeza Omanga.