Raisi Kenyatta na aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Sarai hapo awali. Viongozi mbali mbali wanapinga hatua ya Sarai kujiunga na Jubilee.kenyapoa.wordpress.com
Aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar Sarai amelaumiwa vikali baada ya hatua yake ya kujiunga na chama cha Jubilee.
Wa kwanza kukashifu hatua hiyo ni mbunge wa Likoni, Mishi Mboko, aliyeitaja hatua ya Sarai kama yakujinufaisha kibinafsi na wala si kwa lengo la watu wa Mombasa.
Siku ya Jumapili, Sarai alitangaza rasmi kujiunga na Jubilee kwenye mkutano uliohudhuriwa na raisi Kenyatta na naibu wake katika uwanja wa Serani jijini Mombasa.
Vile vile, Sarai alitangaza kumuunga mkono raisi Kenyatta kwenye marudio ya uchaguzi wa uraisi.
“Nitamuunga mkono Kenyatta kwenye uchaguzi wa marudio na nina imani atapita,”alisema Sarai.
Mboko amewataka wakazi wa Mombasa kutobabaishwa na hatua ya Sarai na kusema kuwa Nasa itashinda kwenye marudio ya uchaguzi wa uraisi.
“Hatubabaishwi, Nasa tuko mbele na tutashinda uchaguzi wa marudio,” alisema Mishi.
Akiwahutubia wafuasi wa NASA kwenye maandamano yao ya kila wiki, mbunge huyo amemtaja Sarai kama mtu aliyekataliwa kisiasa na kusema kuwa kuhama kwake hakuna athari yoyote.
Adiha, Mboko amesisitiza kuwa NASA itasalia kuwa imara katika kaunti ya Mombasa chini ya uongozi wa gavana Hassan Joho.
Naye aliyekuwa mwakilishi wa wanawake kaunti ya Lamu Shakila Abdalla ameshtumu kuhama kwa Sarai kujiunga na chama cha Jubilee.