Hatua ya Wajumbe wa Bunge la Kaunti ya Mombasa ya kutia makonde bungeni imezidi kukosolewa na viongozi wa mbalimbali wa kaunti hiyo.
Seneta wa Kaunti hiyo Hassan Omar Sarai, amezitaja vurugu zilizoshuhudiwa katika bunge hilo la kaunti kuwa aibu kubwa kwa viongozi hao.
Sarai amewalaumu Wawakilishi wa Kaunti hiyo kwa kukosa kupitisha miswada muhimu na kujadili ajenda za maendeleo, akisema tabia hiyo inaonyesha kuwa wameshindwa kuwajibikia majukumu yao.
“Tunashutumu hatua ya Wawakilishi wa bunge la kaunti ya Mombasa kwa kuonyesha kukosa nidhamu kwa umma na kuzibana makonde hatua hiyo imekiuka maadali na katiba,”alisema Sarai siku ya Ijumaa mjini Mombasa.
Kauli ya kiongozi huyo inajiri kufuatia mzozo ulioshuhudiwa hivi majuzi katika Bunge la Kaunti ya Mombasa pale Wawakilishi wa kaunti walipotofautiana kuhusu shinikizo za kumbandua Spika wa Bunge hilo Thadius Rajwayi.