Aliyekuwa Seneta wa Mombasa.Hassan Omar katika hafla ya awali. [Picha/ kenya-today.com]
Jaji anayesikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho ametakiwa kijiondoa kwenye kesi hiyo.Ombi hilo limewasilishwa na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar, kwa madai kuwa Jaji Lydia Achonde wa Mahakama ya Mombasa anapendelea upande wa Joho.Omar kupitia wakili wake Yusuf Abubakar ametaka ombi hilo kusikilizwa kwa haraka ili kutoa fursa kwa Jaji mkuu David Maraga kuteua jaji mwengine kusikiliza kesi hiyo.“Tunataka ombi letu kusikilizwa kwa haraka ili kutoa nafasi kwa Jaji mkuu kuteuwa jaji mwengine ambaye hana upendeleo wowote,” alisema Abubakar.Abubabak amedai kuwa Jaji Achode amekuwa na upendeleo dhahiri kwa upande wa Gavana Joho na kusema kuwa hakuna haki na usawa utakaopatikana kwenye kesi hiyo iwapo jaji huyo ataendelea kuisikiliza.“Tunaohofia kuwa mteja wangu hatapata haki na uamuzi wa usawa kwa sababu kuna upendeleo fulani unaendelea kwenye kesi hii,” alisema Abubakar.Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi wa ombi hilo siku ya Alhamisi wiki hii.Omar aliwasilisha kesi hiyo mahakamani kupinga ushindi wa Gavana Joho kwa madai kuwa uchaguzi wa Agosti 8 haukuwa wa huru na wazi.Tayari zaidi ya mashahidi 20 wametoa ushahidi wao kwenye kesi hiyo.