Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Jr amewakosoa wanaomkashifu Seneta wa Mombasa Hassan Omar, katika azimio lake la kukiwania kiti cha ugavana wa Mombasa, katika uchaguzi ujao.
Mutula alitaja hatua hiyo kama kumnyima Omar haki yake ya kikatiba.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili akiandanama na seneta mwenza, Mutula alisema kuwa Omar kama Mkenya mwingine ana haki kwa mujibu wa katiba kugombea nyadhifa yoyote ya kisiasa nchini, bila kuzingatia maoni ya wanasiasa wengine.
“Wanaomkosoa Omar kwa kutangaza kukiwania kiti hiki cha ugavana wa Mombasa ni waoga. Hawataki kupambana naye kwenye debe,” alisema Mutula.
Kwa upande wake, Omar alisema kuwa tayari ameyafanya maamuzi na kwamba hakuna kitu kitakacho mzuia kugombea kiti hicho.
Alieleza imani yake kuwa wakaazi wa Mombasa watampendelea dhidi ya wawaniaji wengine.
Aidha, Omar ambaye pia ndiye katibu mkuu wa chama cha Wiper, alisema kuwa hatua yake imechangiwa na kutofurahishwa na namna kaunti hiyo inavyosimamiwa chini ya uongozi wa Gavana Hassan Joho.
Baadhi wanasiasa kutoka mrengo wa Cord walimkosoa seneta huyo kwa kuonyesha nia ya kutaka kukiwania kiti hicho, wakihoji kuwa hatua hiyo huenda ikaleta mgongana kwenye mrengo huo, kutokana na kuwa Gavana Joho pia anapania kuutetea wadhifa wake.
Kando na Seneta Omar na Gavana Joho, wengine ambao pia tayari wanakimezea mate kiti hicho ni pamoja na mbunge wa Nyali Hezron Awiti, aliyetangaza azma yake siku Jumapili katika eneo la Changamwe, na mfanyibiashara Suleiman Shahbal, aliyepoteza kwa Gavana Joho katika uchaguzi uliopita.