Seneta wa Mombasa Hassan Omar amewataka viongozi wa mrengo wa NASA kushirikiana ili kuhakikisha wanaingia mamlakani baada ya uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na wanahabari wakati wa kuzindua rasmi zoezi la kuwahamasisha wakaazi kuhusu umuhimu wa kusajiliwa kama wapiga kura linaloendelezwa na chama cha Wiper mjini Mombasa, Omar alisema kuwa ni jukumu la viongozi wa mrengo huo kushirikiana vyema katika utendakazi wao ili kuhakikisha wanaibandua mamlakani serikali ya Jubilee ifikapo mwezi Agosti.Omar amewataka viongozi wa upinzani kuendeleza sera nzuri za kujenga mrengo huo kama njia moja ya kuuimarisha na kuepuka kuwachanganya Wakenya kisiasa.Seneta huyo aidha ameitaka mirengo ya kisiasa humu nchini kuendeleza hamasa zao za kuwaelimisha Wakenya kuhusu jinsi ya kupiga kura na kuasi kuzozana kila siku kuhusu swala la wizi wa kura.Omar aidha alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona idadi kubwa ya Wakenya hawajajitokeza kujisajili kama wapiga kura, hatua aliyoitaja kusababishwa na hamasa duni miongoni mwa wananchi.Wakati huo huo, amewataka Wakenya kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kupata fursa ya kuwateua viongozi watakaotetea maslahi yao.
Maelezo ya picha: Seneta wa Mombasa Hassan Omar akiwahutubia wanahabari katika hafla ya awali.
Picha/the-star.co.ke