Seneta wa Kaunti ya Mombasa amewataka Waislamu katika eneo la pwani kuiombea nchi inapopitia masaibu mbali mbali na misukosuko ya kisiasa, ugaidi, migomo ya walimu pamoja na matumizi ya dawa kwa vijana.
Akiongea siku ya Alhamisi baada ya sherehe za Eid-al-Adha, Seneta Hassan Omar alisema kuwa shida ambazo zinaikumba nchi ya Kenya kwa sasa zinahitaji viongozi wa kidini kushikana mikono na kuiombea nchi ili iweze kuendelea.
Vile vile aliwataka ndugu wa Kiislamu kuendelea kuwafaa wale ambao hawana uwezo wa kifedha kwa kuwasaidia na chakula ili nao waweze kujifurahisha katika siku muhimu za kalenda ya waislamu.
Alisema kuwa yeye pamoja na chama cha upinzani cha Cord wataendelea kupigania haki za walimu hadi seriakli ya Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuwalipa walimu nyongoza yao ya mishahara ilivyoamuru mahakama kuu.
“Serikali ina pesa ya kutosha kuwalipa walimu na nashangaa ni kwa nini serikali imekuwa ikitoa pesa kulipa kampuni kama Kenya Airways and Mumias Sugar lakini za walimu zinakosekana,” alisema Omar.
Omar alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuacha kupotoshwa na kuanza kuchukua ushauri kutoka kwa viongozi ambao wanaitakia nchi ya Kenya mema.
Alisema kuwa bado watajadili ule mswada ambao unalenga kupunguza mshahara wa maafisa katika ofisi za serikali kwa asiliamia hamsini ambao uliandaliwa na mbunge wa Budalangi Ababu Namwamba.