Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar amewahimiza wakaazi wa kaunti hiyo kuwachagua viongozi wasomi.
Seneta Omar aliwahimiza wakaazi kuwachagua viongozi waliosomea nyadhifa mbali mbali za uongozi wa kaunti hiyo kwa kuwa ufisadi uliokithiri katika kaunti nyingi ndio adui mkubwa wa ugatuzi.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano katika hoteli ya Whitesands, Omar alisema kuwa kwa viongozi wote walio kwenye kaunti hiyo, ni yeye tu ambaye vyeti vyake vya elimu havijatiliwa shauku, huku akiwahimiza watu ambao wanataka kua viongozi kwenda shuleni kwanza.
“Kiongozi aliyesoma huwa na maarifa mengi ya kuanzisha miradi mbali za maendeleo. Wale ambao mawazo yao ni ya kifisadi tu hawawezi kufanya maendeleo yoyote,” alisema seneta huyo.
Seneta huyo alitoa changamoto kwa wananchi kuwachagua viongozi kulingana na sera zao na wala sio chama na kuongeza kuwa kuna kaunti nyingi ambazo zimeendelea kwa kuchagua viongozi bora.