Chama cha Wiper kimetoa hakikisho kuwa kitakuwa na mgombea mmoja wa kiti cha ugavana katika Kaunti ya Mombasa.
Seneta wa Mombasa Hassan Omar na Mbunge wa Nyali Hezron Awiti, wote ambao wametangaza azma yao ya kuwania kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu ujao, wameapa kufanya kazi pamoja ili kumng’atua mamlakani Gavana Hassan Joho.
Akizungumza siku ya Alhamisi walipozuru Uwanja Wa Tononoka kukagua matayarisho ya mkutano wa chama cha Wiper, Omar ambaye ni katibu mkuu wa chama hicho, alitoa hakikisho kuwa Wiper iko imara katika Kaunti ya Mombasa.
“Chama cha Wiper kiko imara na ushindani baina yangu na Awiti haufai kuchukuliwa kama uhasama, kwani unaashiria demokrasia katika chama chetu,” alisema Omar.
Kauli ya Omar iliungwa mkono na Awiti ambaye ametoa hakikisho kuwa wameafikia makubaliano kuwa atakayeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho ataungwa mkono na wenzake.
Haya yaniri huku kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka akitarajiwa kuzuru eneo la Pwani kuanzia Jumamosi.
Chama cha Wiper kinanuia kutumia mkutano huo kuendeleza umaarufu wake katika eneo hilo.
Omar alisema kuwa mkutano huo pia utatumiwa kutoa uamuzi muhimu sana kuhusu chama hicho.