Huku uchaguzi mkuu nchini ukikaribia, seneta wa Kaunti ya Mombasa Omar Hassan ametangaza rasmi kuanzisha vuguvugu la mabadiliko ikiwa njia mojawapo ya kutia makali azimio lake la kumbandua gavana wa sasa wa kaunti hiyo Ali Hassan Joho.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio nchini siku ya Alhamisi, Omar amefafanua nia yake ya kuleta mabadiliko kamili kwenye kaunti hiyo huku akiikosoa rekodi ya gavana wa sasa kwa kusema kuwa bado hajafanya wala kutimiza ahadi za kuleta maendeleo kiuchumi kwa wenyeji wa kaunti ya Mombasa.

Seneta huyo alitaja sekta nyingi ambazo zimekwazwa tangu mamlaka ya sasa kuchukua hatamu ya uongozi na kutoa mfano wa sekta ya biashara kuwa chini kwa sababu ya kodi ilio juu na ukosefu wa uwazi pamoja na uhusishwaji usio wa moja kwa moja kwa washika dau kwenye sekta husika.

Japokuwa seneta Omar aliweza kuzitambua baadhi ya sehemu ambazo gavana Joho amezishughulikia kama vile kurembesha mji na sekta ya ukaguzi, hakusita kuweka wazi wazi kuwa mapungufu ya uongozi wa gavana Joho ni mengi kuzidi manufaa ambayo amewaletea wakazi wa Mombasa kwa muda wa miaka mitatu ambayo amehudumu.

Kwa mtazamo wa seneta Omar, ni sharti aweke mikakati timamu na vuguvugu ambalo litatoa mwelekeo wa sawa ili kuona kuwa kuna maendeleo imara kwenye jiji hilo la pili nchini kwa viwango vya uchumi kwenye eneo hili.

Omar Hassan anaungana na wengi wa maseneta nchini ambao wametangaza nia ya kuwania ugavana mwaka wa 2017 kama vile Bon Khalalwe (Kakamega), Mike Sonko (Nairobi), Kiraitu Murungi (Meru) miongoni mwa wengine.