Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar Sarai ameupinga mradi wa serikali ya kaunti ya Mombasa wa kuzibomoa nyumba za wakaazi wa kaunti hiyo na kuziboresha, akidai kuwa ni njama ya kaunti hiyo kuwauzia nyumba hizo wawekezaji wa kibinafsi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumapili, Sarai amesema kuwa hakuna mtu yeyote atakayeweza kuuza nyumba za wakaazi licha ya kuwa zinamilikiwa na kaunti ya Mombasa huku akisema kuwa lazima ugatuzi kuzingatiwa, na kuitaka serikali ya kaunti hiyo chini ya uongozi wa Gavana Joho kusitisha mpango huo mara moja.

Sarai amesema kuwa jukumu la kaunti ni kuwapa wakaazi mazingira bora na wala sio kuwahangaisha kwa lengo la kuwauzia wawekezaji wa kibinafsi nyumba hizo na kusema kuwa kama viongozi hawatakubali mradi huo kutekeleza Mombasa.

“Kama viongozi hatutakubali wakaazi wakiondolewa kwenye nyumba hizo hata kama zinamilikiwa na serikali ya kaunti ya Mombasa kwa sababu nyumba hizo ni za watu walio na kipato cha chini kuishi hapo, sasa mkiwafurusha mnatarajia waende wapi? hilo sisi hatutakubali,” alisema Sarai.

Wakati uo huo, amewataka wakaazi wanaoishi katika nyumba hizo kutokubali kuhama hadi swala hilo kutatuliwa kwani hatua ya serikali ya kaunti ya Mombasa kuwafurusha wakaazi hao ni ukiukaji wa ugatuzi, huku akiwaonya maaskari wa kaunti kukoma kuwahangaisha wakaazi.

Awali, serikali ya kaunti ya Mombasa ilitangaza kutenga shilingi bilioni 200 kuzibomoa nyumba za makaazi ya maeneo ya Buxton, Likoni, Khadija, Changamwe na Tudor na kuzijenga upya nyumba hizo ili kuboresha mji wa Mombasa, hatua ambayo imepingwa na wakaazi wengi Mombasa.