Huenda Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar akijipata taabani baada ya kuushtumu Mrengo wa Cord na Kinara wake Raila Odinga kuhusu uongozi wa Mombasa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mshirikishi mkuu wa Chama cha Wiper Kaunti ya Mombasa Afiya Rama amesema kuwa lazima seneta huyo kuomba msamaha kwani matamshi aliyoyatoa siku ya Jumamosi ni uchochezi na huenda yakavuruga chama hicho nchini.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, Afiya alisema kuwa viongozi wa mrengo wa Cord wanahitaji kuwa na ushirikiano na iwapo malumbano ya kisiasa yatazidi kushuhudiwa, basi huenda mrengo huo ukavunjika.

Rama alisema kuwa iwapo Senator Omar ana azma ya kuwania ugavana wa Kaunti ya Mombasa wakati wa uchaguzi mkuu, basi hapaswi kuwagonganisha Wakenya na wanachama wa mrengo huo, hususan chama cha Wiper.

Rama alisema kuwa huenda Omar akabanduliwa kama katibu wa chama cha Wiper nchini iwapo ataendelea na mkondo huo.

"Kila Mkenya ana haki kikatiba kuwania uongozi anaouenzi lakini sio kuwachochea watu wengine. Hatutakubali hatua hiyo kama wanachama wa chama cha Wiper kutoka Mombasa,” alisema Afiya.

Kauli ya kiongozi huyo inajiri baada ya Omar kusema kuwa kinara wa mrengo wa Cord Raila Odinga anaingilia siasa za Mombasa.