Malumbano yanayoendelea kushuhudia mjini Mombasa baina ya Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho na Mshirikishi mkuu wa Utawala eneo la Pwani Nelson Marwa huenda yakaathiri zaidi maendeleo katika kaunti ya Mombasa.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar amesema kuwa mgogoro huo umechangia pakubwa kubadilisha msimamo wa wakazi kushinikiza kupewa huduma bora zaidi ikiwemo Afya, Elimu, Muundo msingi na Maji.
Omar amesema kuwa asilimia kubwa ya shughuli za kibiashara katika kaunti hiyo zimeshuka zaidi na huenda uchumi wa kaunti hiyo ukadodora, huku akitaka uhasama huo kusitishwa ili kuwasaidia wakazi kuwatekelezea maswala muhimu yanayoboresha maendeleo ya kaunti hiyo.
"Uhasama baina ya Joho na Marwa umeshuhudiwa mara kadhaa, na iwapo hautapata suluhu, basi kaunti ya Mombasa itarudi nyuma kimaendeleo kwani imechangia wakazi kushindwa kushinikiza kutekelezwa kwa shughuli muhimu za kimaendeleo," alisema Omar.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Kamanda mkuu wa polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi kushinikiza kuwa sharti Joho asalimishe bunduki zake, la sivyo akabiliwe na mkono wa sheria.
Uhasama baina ya Joho na Marwa umeshuhudiwa mara kadhaa, huku Seneta akidai kuwa Marwa amepewa mamlaka na Serikali kupita kiasi.
Picha: Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar. Amesema kuwa uhasama baina ya Joho na Marwa umechangia maendeleo duni ya kaunti. Maktaba