Msemaji wa kanisa la Katoliki katika kaunti ya Kisii Jeremiah Nyakundi amewaomba Wakenya wote kuombea serikali ya kitaifa na zile za kaunti ili taifa la Kenya lisonge mbele kimaendeleo.
Nyakundi alisema maombi ndio yatasaidia serikali hizo pamoja na viongozi ili kuwa na maarifa ya kuongoza Wakenya na kufanya maendeleo.
Akizungumza siku ya Jumapili katika kanisa la Katholiki lililoko mjini Kisii, Nyakundi alisema maombi ndio suluhisho kwa kila jambo na kusema kuna haja kwa wakenya kujiunga pamoja ili kuombea viongozi wa taifa.
Aidha, aliomba bodi mpya ya mitihani nchini KNEC kuombewa ili kufanya kazi vilivyo na kuwapa wanafunzi haki zao wanapofanya mitihani nchini.
Nyakundi alimpongeza waziri wa elimu Matiang’i kwa kuvunjilia mbali bodi ya zamani ya KNEC kwa kile ilichodaiwa kuhusika katika visa vya udanganyifu .
“Naomba Wakenya wenzangu tuweke maombi ya kutosha kwa serikali zetu ili kusonga mbele na tuombee bodi mpya ya KNEC ili wanafunzi wa Kenya wapate haki katika mitihani yao kila mwaka,” alisema Nyakundi .