Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amewataka wakenya kuwaombea magavana wote nchini pamoja na serikali za ugatuzi kutokana na mizozo inayoshuhudiwa katika baadhi ya kaunti nchini.
Akiongea ijumaa wakati wa baraza la umma katika mji wa Njoro, Mbugua alisema kuwa kuna shetani wa kisirani na mizozo ambaye amevamia serikali za ugatuzi na kuzua hali ya kutoelewana.
Mbugua alisema kuwa ni muhimu wakenya waombe mwenyezi mungu awalinde magavana na alete hali ya kuelewana kati ya viongozi katika kaunti.
“Kuna tatizo la kutoelewana kati ya viongozi katika baadhi ya kaunti zetu na ni muhimu nyinyi kama wananchi muwakumbuke viongozi wote kaunti zote katika maombi yenu ili mwenyezi mungu atuepushane na balaa ya mizozo kila mara. Tuna bahati kuwa hapa kwetu Nakuru huyo shetani hajatuvamia lakini ni vyema tuzidi kuombea wenzetu wa Makueni, Machakos na Narok ili warejelee hali ya kawaida,” alisema Mbugua.
Mbunge wa Njoro, Joseph Kiuna kwa upande wake aliwataka magavana kuwa na moyo wa majadiliano ili kuepusha mizozo kama ile inayoshuhudiwa Machakos, Narok na Makueni.
“Matatizo mengi yanayoshuhudiwa katika kaunti yanaweza kutatuliwa kwa njia rahisi iwapo magavana kama wakuu wa kaunti watakuwa katika mstari wa mbele kuhimiza mazungumzo baina ya viongozi kwa maana hapatakuwa na maendeleo iwapo viongozi watazidi kuzozana kila wakati,” alisema Kiuna.