Ombi la kuwafungulia mashtaka upya wasichana wanne wanaokabiliwa na mashtaka ya ugaidi limepingwa na Hakimu Simon Rotich katika mahakama ya chini jijini Mombasa.
Akitoa uamuzi wake siku ya Jumanne, Hakimu Rotich alisema kuwa hawezi kulikubali ombi hilo lililowasilishwa na afisi ya mashtaka ya umma hadi pale atakaposkiza upande wa utetezi.
Upande huo wa utetezi ulikuwa umepinga kusomewa mashtaka kwa wateja wao huku wakishikilia kuwa nakala mpya ya mashtaka iliyonuiwa kutumika ni sawa na ya hapo awali.
Mwendesha mashtaka Daniel Wamota alisema kuwa baada ya uchunguzi, waliwapata na mashtaka zaidi ya kujibu.
Wanne hao walifikishwa katika mahakama hiyo ya Mombasa kuskiza kesi hiyo na watasalia kizuizini licha ya kupewa dhamana ya Sh500,000 kila mmoja.
Khadija Abdikadir, Halima Ali, na wenzao wawili walikamatwa mapema mwaka huu katika eneo la Elwak, kaunti ya Wajir, kwa madai ya kuelekea nchini Somalia kujiunga na kundi la al-shabaab.
Kesi hiyo itaskizwa tena tarehe Desemba, 24.
Kwengineko, katika mahakama hiyo ya Mombasa, Shahidi wa kwanza katika kesi inayowakabili watu watano wanaoshukiwa kuvamia kambi ya wanajeshi eneo la Nyali mwaka jana ametoa ushahidi wake mbele ya Hakimu mkuu Richard Odenyo.
Solomon Onyango, afisa aliyekuwa akishika doria usiku wa tukio alisimulia mahakama jinsi kundi la vijana zaidi ya 20 walivyovamia kambi hiyo wakiwa wamejihami kwa panga, visu na hata chupa za petroli.
Akitoa ushahidi wake, Onyango alieleza kuwa tukio hilo lilipelekea kifo cha afisa mmoja na wengine kujeruhiwa huku bunduki moja iliyokuwea na risasi 30 kuibiwa.
Akihojiwa na mwendesha mashtaka Simon Waithaka, shahidi huyo alisema kuwa lengo la wavamizi hao lilikuwa ni kuiba bunduki kutoka kwa maafisa waliokuwa wakishika doria katika kambi hiyo.
Hata hivyo wavamizi zaidi ya watano waliuawa katika shambulizi hilo.
Washukiwa wa uvamizi huo Mohammed Moye, Ali Hamisi na wengine watatu wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji na wizi wa mabavu huku shahidi huyo akikiri kutowatambua kutokana na kuwa walikuwa wamejifunga vitambaa usoni wakati wa uvamizi.
Kesi hii inatarajiwa kuwa na mashahidi wanne na itaendelea siku ya Jumatano.