Wanakandarasi wa kukarabati barabara na kuweka miradi ya maji katika wadi ya Sensi eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini wamehimizwa kuharakisha kandarasi zao ili wakaazi wa wadi hiyo waanze kufaidi.
Wito huo umetolewa baada ya wanakandarasi hao kuchukua muda mrefu tangu wakabidhiwe kandarasi hizo katika bajeti ya mwaka 2013/2014.
Akizungumza siku ya Jumapili Mwakilishi wa wadi ya Sensi Onchong’a Nyagaka alisema wanakandarsasi hao wamechukua mda mrefu huku wakaazi wakiteseka kupita katika barabara za eneo hilo ambazo ni mbovu.
“Kuna kandarasi ambazo bado hazijakamilika katika wadi yangu tangu mwaka wa 2013 na wanakandarasi ni kama hawawajibiki katika kazi zao," alisema Nyagaka.
"Nawaomba wajaribu kila wawezalo kuhakikisha kazi walizokabidhiwa wamezimaliza,” aliongeza Nyagaka.
“Miradi ya maji bado haijaanza kutengenezwa na tayari kuna wanakandarasi ambao walipewa kazi hiyo lakini bado hawajaanza hiyo kazi," alisema Nyagaka.
"Wakaazi wa wadi yangu wameteseka zaidi kutokana na miradi kutokamilika ambayo ni kwa manufaa yao,” aliongeza Nyagaka.