Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kuwajengea wakazi wa eneo la Daraja Mbili daraja baada ya wakazi hao kuandamana siku ya Alhamisi, wakilalamikia kuharibika kwa daraja lililoko katika eneo hilo ambalo limesababisha vifo vya wenyeji.
Wandamanaji hao ambao walikuwa wamebeba jeneza la mkazi ambaye alifariki alipokuwa akivuka daraja hilo, walizuiliwa katika lango kuu la kuingia katika afisi za bunge la kaunti ya Kisii, ambapo walitaka kuhutubiwa na Gavana Ongwae.
Gavana Ongwae aliwaambia kuwa atawajengea daraja la chuma kwa muda wa miezi mitatu na kuongeza kuwa atawashauri maafisa husika kwenye idara ya miundomsingi ya kaunti hiyo kuweka daraja la mbao ili wakazi wawe wanaitumia wakisubiri ujenzi huo kukamilika.
“Nimesikia kilio chenu na nimemwagiza mhandisi katika idara husika kuharakisha ujenzi huo wa daraja la chuma. Nataka mtengenezewe ile ya mbao mwendelee kuitumia katika muda huu ambao mtakuwa mnangojea ile ya chuma kukamilishwa,” alisema Gavana Ongwae.
Mmoja wa wakazi kutoka eneo hilo, Elvis Omeka alisema wameshuhudia visa vingi vya watu kusombwa na maji kufuatia kufurika kwa maji katika mto mmoja ambao unapita katika eneo hilo.
“Zaidi ya watu wanane wameaga dunia, ndio sababu tuliamua tuandamane hadi kwenye ofisi ya gavana atafute utatuzi wa suala hili ambalo linaendelea kumaliza wakazi. Tumefurahi kwa sababu gavana wetu ametuahakikishia kuwa daraja litajengwa,” alisema Omeka.