Kama njia mojawapo ya kuufanya mji wa Kisii kuwa na mpangilio unaofaa na ambao unaruhusu watu pamoja na waendeshaji magari kupita bila vizuizi, kaunti ya Kisii imeweka mikakati ya kuona kuwa kila sehemu inapewa steji yake ili kuepusha madereva wa matatu kuegesha magari yao kiholela.
Katika ziara ya siku ya Jumatano ya kukagua miradi, biashara, kuangalia uratibu wa majengo na vituo vya magari vilivyopangwa mjini Kisii, gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae alisema kuwa anaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa steji za magari ya abiria zitawekwa kulinganana na sehemu magari yanahudumu.
Ongwae alisikitikia msongamano uliopo, hali ambayo alitaja kuwa huenda ikaleta changamoto nyingi katika sekta ya matatu kwa vile itakuwa vigumu kwa wengi wa wahudumu pamoja na abiria kupitisha mizigo yao na hufanya wasafiri wengi hata kuhisi hofu ya kukosa usalama.
“Kila eneo linapaswa kuwa na steji yake ili kupunguza msongamano kutoka katikati ya mji, lakini pia shida iliopo ni kuwa ardhi ndogo ambayo haitatosheleza shughuli nzima,” Ongwae alisema.
Hata hivyo, gavana alitaja ukosefu wa ardhi kuwa chanzo kikubwa cha kutofanikisha miradi kama hiyo, lakini akahidi kuwa atafanya kila awezalo kuona mji wa Kisii uko katika mpangilio unaovutia na wa kupitika na magari pamoja na watu.