Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amesema hajaridhika jinsi maendeleo yamefanywa katika kaunti yake, na kuhaidi kuwa atahakikisha kuwa maendeleo zaidi yamefanywa kwa wananchi wa kauti hiyo
Akizungumza mnamo siku ya Jumatatu na waandishi wa habari afisini mwake, Ongwae alikiri kuwa hajaridhika na utendakazi wa serikali yake, haswa yale alivyowahidi wananchi wakati wa kampeini.
Ongwae aliwataka maafisa wa kaunti hiyo kufanya maendeleo zaidi, huku wakitumia pesa za serikali ya kaunti hiyo vizuri ili kuafikia matarajio yake kwa maendeleo kabla ya kura zijazo.
“Sijaridhika na kiwango cha maendeleo katika kaunti yangu ila nitashirikiana na maafisa wangu ili tuhakikishe maendeleo niliyowahidi wananchi nimeyatimiza vilivyo,” alihoji Ongwae.
Ikumbukwe kuwa kauti ya Kisii iliorodheshwa kuwa ya nne kwa maendeleo kote nchini,na serikali hiyo kusema itajaribu kila iwezalo kuhakikisha kuwa ya kwanza katika maendeleo mbalimbali.
Kwa upande mwingine, wakaazi wa kaunti hiyo walifurahishwa jinsi amefanya maendeleo katika kaunti hiyo, haswa kwa kukarabati baadhi ya barabara, kuweka mataa katika masoko, kukarabati baadhi ya chemichemi za maji.
Wakaazi hao wamemtaka gavana kuzungumza na wawakilishi wa wadi za kaunti yake kukarabati barabara kikamilifu ili kuwaridhisha kimaendeleo.
“Mimi natoka wadi ya Sengera Bosoti na ninaona kiwango cha ukarabati wa barabara za eneo la wadi hiyo uko nchini sana haswa katika barabara ya Kineni, naomba Ongwae kumwamuru mwakilishi wetu kutukarabatia barabara kikamilifu,” alisema George Simba, mkaazi.