Gavana wa kaunti ya Kisii Bw James Ongwae amewataka walimu wakuu wa shule za upili kusaidia kutambua wanafunzi walio na mahitaji maalum ili wapewe msaada wa kifedha wa karo kutoka kaunti.
Ongwae alisema hii ni moja ya hatua muhimu serikali ya kaunti ya Kisii imechukua kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi ambaye analengwa na msaada huu, wakiwemo mayatima na watoto kutoka familia maskini, anafikiwa na kusaidika kulipa karo.
Kwenye hotuba yake ofisini mwake mjini Kisii kwenye kikao na walimu wakuu wa Shule za upili Alhamisi, gavana Ongwae alitoa wito kwa walimu hao kumuunga mkono kwenye harakati ya kuhakikisha masuala ya elimu yanafaulu.
Hii itawezekana kwa kutambua kila mwanafunzi asiye na uwezo wa kulipa karo ili watume maombi ya msaada wa pesa za maendeleo ya eneo bunge CDF na zile za ufadhili kutoka kaunti.
"Tuwape kipaumbele wale wasio na wazazi, familia maskini na wale wa mahitaji maalum ili kupunguza visa vya wengine kuacha shule kwa kukosa karo," alisihi gavana Ongwae.
Gavana aliwahidi walimu hao wakuu kuwa atajitahidi vilivyo ili kuona eneo la Gusii linabobea kwa masuala ya elimu.