Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae ameombwa kuwajumuisha vijana katika ajira pamoja na shughuli zingine za maendeleo katika serikali yake ya kaunti.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wengi wa vijana hawajajumuishwa kikamilifu kwa serikali ya kaunti hiyo, jambo ambalo vijana wanalitaka kuangaliwa na kuzinagatiwa kikamilifu.
Wakiongea siku ya Jumatano mjini Kisii, vijana hao, wakiongonzwa na Cornelius Ombae walisema kuna idadi kubwa ya vijana katika kaunti hiyo ambao wamehitimu katika taaluma mbalimbali, lakini bado hawajapata ajira kwa serikali ya kaunti hiyo.
“Tunaiomba serikali ya kaunti yetu ituhusishe sisi vijana maana wengi wetu tuko na ujuzi lakini hatujawahi pata fursa ya kutumia ujuzi wetu tulioupata shuleni ili kutumia kwa serikali yetu ya Kisii au kwa mashirika mengine,” alisema Janet Morema, mmoja wa vijana hao.
“Tayari mimi nimekuwa nikijaribu sana kutafuta ajira katika kaunti hii ya Kisii lakini sijawahi fanikiwa. Kama wazaliwa wa hapa, tunaomba serikali ya kaunti ituhusishe sisi vijana na kutupa ajira,” alisema Shem Maiko, kijana mwingine.
Aidha, vijana hao waliomba vijana wengine kuungana pamoja na kuchukua mikopo ya serikali ya kaunti ili waweze kujiimarisha na kujiendeleza kimaisha, kwani imeonekana hakuna matumaini ya kupata ajira katika afisi.
“Tutaendelea kuomba vijana wengine wale hawakujumuika nasi leo waungane na kuchukua mikopo ya kuanzisha biashara ili tujitegemee na tuinue uchumi wetu,” aliongeza Maiko.