Gavana wa kaunti ya Kisii amewaonya wafanyikazi wa kaunti dhidi ya kuzembea kazini na kusema iwapo hawatatia bidii watafutwa kazi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiongea katika uwanja wa Gusii siku ya Jumatatu, wakati wa kuadimisha siku ya Madaraka, gavana James Ongwae alisema mswada wa maadili ya wafanyikazi wa kaunti umetayarishwa na utaanza kutumika baada ya kupitishwa na bunge la kaunti.

Gavana Ongwae alimtaka spika wa bunge la kaunti kuharakisha katika kupitisha miswada muhimu ili kuharakisha utendakazi wa kaunti.

“Kuna mswada ambao unaendelea kushughulikiwa na pindi tu utakapokamilika, tutautoa na utaanza kufanya kazi na wale watakaopatikana wakizembea kazini na kujihusisha na maswala ya ukosefu wa utovu wa nidhamu, watapoteza kazi zao,” alisema Ongwae.

Kwa upande wake, naibu wake Joash Maangi aliwaonya wafanyikazi hao dhidi ya kujihusisha na siasa na kuwaambia huenda wakapoteza kazi zao iwapo wataendelea na siasa.

“Kunao wafanykazi wa kaunti ambao wanaojihusisha na siasa badala ya kuwatumikia wakaazi wa Kisii. Ningependa kuwaonya kuwa mtapoteza kazi zenu iwapo mtaendelea na siasa,” alionya Maangi.

Maangi aliwaonya wanakandarasi dhidi ya kupiga foleni huku wakidai malipo bila kufuata njia mwafaka.

“Wanakandarasi hushinda siku nzima katika afisi za ‘Treasury’ wakitaka kulipwa pesa zao. Sio vibaya lakini mnafaa kuelewa na kujua njia mwafaka ya kufuata hela zenu badala ya kupoteza siku nzima ilhali mungekuwa mumefanya kazi,” alisema Maangi.