Wakazi wa eneo la Kisii wameombwa kuwa mbali na mahali pa mkasa ili kuzuia maafa zaidi na kutoa nafsi mwafaka kwa maafisa wa polisi na wahudumu wa msalaba mwekundu kuwaokoa manusura.
Akiongea siku ya Jumapili katika Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii alipowatembelea walionusurika kifo kutokana na ajali mbaya ya barabara iliyotokea eneo la Ogembo, Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae aliwaomba wakazi wa Kisii kuwa mbali na mahali mkasa umetokea ili kuzuia maafa mengine.
Haya yanajiri baada ya ajali kutokea katika eneo la Ogembo Jumapili na nyingine katika sehemu iyo hiyo baadaye wakati wakazi walikuwa wamekushanyika katika maeneo hayo na kusababisha vifo vya watu wawili zaidi.
“Naomba wakazi wote kuwa mbali wakati mkasa au ajali imetokea kama njia moja ya kuzuia na maafa mengine zaidi," alihoji Gavana Ongwae.
Gavana Ongwae alisema wakazi wakiwa mbali na mkasa itawasaidia hata maafisa wa polisi na wahudumu wa msalaba mwekundu kuwaokoa watu kutoka kwa mkasa huo.
Aidha, alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii itawashughulikia wale waliopata majeraha kutokana na ajali hiyo na kugaramia mazishi ya wale waliofariki kutokana na ajali hiyo.
Gavana huyo pia aliwaomba madereva na wahudumu wa bodaboda kuwa waangalifu na kutoendesha gari kwa kasi sana kwani ajali hizo husababishwa na wanaoendesha kwa mwendo wa kasi.