Gavana wa Kisii James Ongwae amewataka vijana kujiunga na vyuo vya anuwahi na kutupilia mbali kasumba kuwa vyuo hivyo ni vya walioanguka mitihani, na kuahidi kufufua vyuo vyote vilivyomo katika kaunti hiyo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

akiongea na waandishi wa habari jana katika vyuo vya anuwahi vya Nyaore na Nyamondo ambapo walikuwa wameandamana na mbunge wa Nyaribari Chache Central Bwa Momoima Onyonka, Gavana Ongwae alisema kuwa atajitahidi kuona kuwa vyuo hivyo vimekarabatiwa na kutiwa vifaa vinavyohitajika ili kuwafaa wanafunzi.

“Vyuo vya anuwahi vimekuwa vikififia pole pole, kwa hivyo tumechukua hatua ya kuanza kuvishughulikia kwa kuvianzisha upya ili wale wanataka kujiunga wanufaike navyo,” alisema Ongwae.

Pia aliwataka wazazi na vijana ambao walifanya mtihani wa darasa la nane na kidato cha nne kukumbatia taaluma inayotolewa na vyuo kama hivyo, na kujiandikisha ili kupata ujuzi na taaluma ya kiufundi.

“Nawaomba vijana wote kuja katika vyuo hivi na kujiandikisha katika taaluma wanayopendelea ili kujipa utaalamu wa kiufundi, na mwache kudharau vyuo hivi,” gavana Ongwae aliwasihi vijana.

Naye mbunge wa eneo hilo Momoima Onyonka, ambaye alikuwa ameandamana na Ongwae aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo kuwa watafanya kazi pamoja kwa ushirikiano wa kaunti ili kuona vyuo vyote vya anuwahi vinafufuliwa, na kuwasaidia wanafunzi ambao wamekosa nafasi katika taasisi nyingine za elimu.

“Nitafanya kazi na gavana wetu ili kuboresha maisha ya vijana wetu kiulemu, na nitafadhili wanafunzi ambao wana ari ya kuendelea zaidi ya hapa,” alisema Momoima.