Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameahidi kufungua kituo kipya cha magari katika Soko la Daraja mbili mjini Kisii.

Ongwae alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa sababu magari ya umma yameongezeka mjini Kisii na husababisha misongamano mikubwa ya magari.

Akizungumza siku ya Ijumaa mjini Kisii, Ongwae alisema tayari mikakati ya kukifungua kituo hicho imekamilika huku akisema kile kinachosalia ni ujenzi kuanza rasmi.

Gavana huyo alisema kuwa ujenzi huo utangoa nanga rasmi Januari mwaka ujao na kuongeza kuwa anatumai kuwa kituo hicho kipya kitakachojengwa kilomita moja tu kutoka mji wa Kisii kitasaidia kupunguza misongamano ya magari ambayo inaendelea kushuhudiwa kila wakati.

Aidha, Ongwae alisema magari ya umma kutoka maeneo ya Nyachege, Tabaka, Ogembo na maeneo mengine ambayo yataratibiwa yatakua yakitumia kituo hicho cha Daraja mbili.

“Tutajenga kituo cha magari mwaka ujao katika soko la Daraja mbili ili tupunguze misongamano ya magari mjini Kisii,” alisema Ongwae.

Aidha, Ongwae alisema sekta ya uchukuzi itaimarika zaidi kufuatia uamuzi wa mahakama kuwa sekta hiyo iwe chini ya usimamizi wa serikli za kaunti.