Magavana wa kaunti za Kisii na Nyamira wameombwa kuheshimu mkataba wa maelewano uliotiwa sahihi kwa upamoja na kumaliza mzozo ulioko katika mpaka wa Keroka.
Hii ni baada ya mzozo wa mpaka huo wa Keroka kuendelea kushuhudiwa kila wakati huku ukusanyaji ushuru katika soko hilo ukikumbwa na changamoto si haba.
Mpaka huo unatenganisha kaunti hizo mbili lakini wakusanyaji ushuru wa kaunti hizo mbili huwa wanavuka mpaka na kutoza ushuru sehemu ya kaunti ingine bila kibali, jambo linaloleta malumbano.
Kulingana na mbunge wa Nyaribari Masaba, kaunti ya Kisii, Elijah Moindi aliyezungumza na mwandishi huyu, aliomba magavana James Ongwae na mwenzake John Nyagarama kuheshimu mkataba wa maeleawano uliotiwa sahihi ili kumaliza mzozo huo.
“Wabunge wa Kisii na Nyamira tulikuja pamoja na tukaelewana mahali ukusanyaji ushuru unatozwa kwa kila kaunti, lakini haya mengine yanendelea hatujui, naomba heshima ionyeshwe na magavana wasuluhishe hayo,” alisema Moindi.