Share news tips with us here at Hivisasa

Magavana wa Kaunti za Kisii na Nyamira wameombwa kuja pamoja na kusuluhisha mzozo wa mpaka wa kaunti hizo mbili, haswa katika soko la Keroka.

Hii ni baada ya vurugu na ghasia kuzuka siku ya Alhamisi katika soko hilo la Keroka na kuwalazimisha maafisa wa polisi kuingilia kati ili kutuliza vurugu hizo.

Vurugu hizo zilianza baada ya maafisa wa kukusanya ushuru wa Kaunti ya Nyamira na wale wa Kaunti ya Kisii, kuonekana kutofautiana kwa ukusanyaji ushuru katika soko hilo, baada ya soko hilo kukubaliwa kuwa chini ya uongozi wa kaunti hizo mbili.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika soko hilo, wafanyibiashara hao wakiongozwa na Patrick Mose na Victor Onsarigo waliomba Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae na Gavana wa Nyamira John Nyagarama kuweka mpaka halisi katika soko hilo, ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Wafanyibiashara hao walidai kutozwa ushuru mara mbili kwa siku, na maafisa wa kukusanya ushuru wa Kaunti ya Nyamira na wale wa Kaunti ya Kisii.

“Tunaomba magavana wetu wakubaliane na kuweka mpaka katika soko la Keroka ili tujue ni sehemu ipi inastahili kuwa kaunti ya Nyamira, na ni ipi iko katika Kaunti ya Kisii,” alisema Mose, mfanyibiashara.

Wafanyibiashara hao walisema kuwa kuwekwa kwa mpaka halisi katika soko hilo kutafanikisha maendeleo.