Mbunge wa eneo bunge la Bomachoge Borabu Joel Onyancha amewaomba walimu wote wa shule za msingi na za upili kuweka motisha na kuhakikisha wanafunzi wanapita katika mitihani yao.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika shule ya msingi ya Ekerubo iliyoko eneo bunge lake katika hafla ya mkutano wa walimu wakuu wa shule za msingi na wanakamati wa shule hizo, mbunge huyo alisema sharti walimu wasomeshe watoto kwa bidii na kuwa na motisha wa kutosha ili wanafunzi wafanye vyema.
Aidha, mbunge huyo alisema wazazi husubiri kuona watoto wao wamefanya vyema, huku akisema bila motisha watoto hawatapita kamwe.
“kila mwisho wa mwaka tunahitaji kuona ni nini mtavuna kama walimu wa shule, na kila mzazi anahitaji kuvuna kile alichotarajia kutoka kwa mtoto wake, hivyo nawaomba kuwasomesha watoto kwa bidii,” alisema Onyancha.
“Naomba walimu msinikasirishe kwa masomo, mjaribu wanafunzi wapite katika mtihani, hata wakulima wa majani chai huvuna baada ya mwaka kukamilika kwa kupokezwa pesa za bakshishi hali maarufu ‘bonus’, nasi sharti tuvune kwa masomo,” aliongezea Onyancha.
Mbunge huyo aliahidi kushirikiana na washkadau wa shule ili kuinua viwango vya masomo.