Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Richard Onyonka, amesema pesa zilizotegewewa magavana, wabunge na wawakilishi wa wadi kwa ziara zitumike kuwalipa walimu mshahara.
Onyonka alisema pesa hizo za ziara hazina faida yoyote ila viongozi kutembea bila manufaa kwa mwananchi wa kawaida, huku akiongezea kuwa ikiwa kiongozi anataka kuwa na ziara, atumie pesa zake.
Akizungumza siku ya Jumapili mjini Kisii, mbunge huyo alisema pesa serikali haitakosa pesa za kuwalipa walimu na kuomba pesa zile hutengwa kwa viongozi haswa za ziara, ziondolewe ili walimu walipwe nyongeza ya mshahara na kuendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi.
“Serikali ina pesa nyingi na ninaomba pesa zile tunatengewa kama viongozi kutembea katika nchi za nje, kununua maua kwa ofisi hazisaidii vyovyote kwa wananchi. Pesa hizo zinastahili kuondolewa na walimu walipwe ili watoto wetu waendelee kusoma na waje kujisaidia nyakati zijazo,” alisema Onyonka.
Mbunge huyo pia aliomba tume ya kuajiri walimu nchini TSC kutoa pesa zile ambazo tayari wamekabidhiwa na serikali kuu ili kuwalipa walimu huku mbinu ya kuendelea kuwalipa walimu ikiendelea kutafutwa.
“Tume ya kuajiri walimu ina pesa. Ndio maana ninaomba tume hiyo itumie ilizonazo kwanza ili walimu waende shuleni kisha tutaona hizo zingine jinsi zitapatikana,” alisema Onyonka.