Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Nyaribari Chache Richard Tong’i na mwezake wa Kitutu kusini Richard Onyonka wametamaushwa na mtindo ambao viongozi serikalini wanavyofuja pesa za umma.

Wakiongea mjini Kisii katika hafla ya kutia sahihi kandarasi ya utendakazi baina ya waziri wa serikali ya kaunti hiyo na gavana James Ongwae, viongozi hao walishinikiza waziri wa ugatuzi Ann Waiguru kujiuzulu mara moja ili uchunguzi ufanywe.

Onyonka alisema kwamba serikali ya Jubilee ni kama imeshindwa na kazi, na wao kama mrengo wa CORD wako tayari kuongoza serikali isiyokuwa na ufujaji pesa kama inavyoshuhudiwa.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, ubadhirifu mkubwa wa fedha umeshuhudiwa katika wizara ya ugatuzi, ambapo zaidi ya bilioni tano huenda umefujwa hadi sasa, huku ufujaji wa haina hiyo ukishuhudiwa katika bunge la kitaifa ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.5 imeibwa na watu wasiojulikana huku akiongeza kuwa katika idara ya usalama wa ndani nchini bilioni 3.5 imeweza kufujwa.

Kwa upande wake, Richard Tong’i ambaye ni mbunge kutoka mrengo wa Jubilee alisisitiza kwamba ni wazi kuwa ufisadi upo serikalini huku akihimiza waziri Waiguru kutoa nafasi ili uchunguzi ufanyike.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na naibu gavana Joash Maangi, spika wa bunge la kaunti ya Kisii Kerosi Ondieki, mawaziri wa kaunti hiyo pamoja na wawakilishi wa wadi miongoni mwa wengine.