Mwaka wa 2010 ulikuwa mwaka wa fursa ya kipekee kwa kila mwananchi nchini Kenya baada ya kujinyakulia katiba mpya iliyotoa nafasi sawa na kuhimiza kila mwananchi kuhusishwa kwenye maafikiano ya maendeleo mbali mbali.
Kupitia katiba hiyo, wananchi wanaoishi na ulemavu walitunukiwa haki za kupata elimu sawa na wananchi wengine, usawa wa nafasi za kazi, haki za kujumuika na kuwakilishwa pamoja na kushiriki katika nyanja tofauti kama vile za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Kwa sasa, haki hizi zimekuwa kinaya kikubwa miongoni mwa wanaoishi na ulemavu katika eneo la Pwani na hata Kenya nzima kwa jumla.
Wanafunzi wanaoishi na ulemavu wamekuwa wakihangaika pakubwa katika hali ya kupata elimu, huku shule kadhaa za walemavu katika Kaunti ya Mombasa zikiendelea kupata idadi kubwa ya wananfunzi ikilinganishwa na vifaa vya kutoa mafunzo kwa wanafunzi hao.
Shule ya walemavu ya Mombasa ni mojawapo ya shule tajika katika kanda ya Pwani, inayojulikana kwa utoaji wa elimu kwa wanaoishi na ulemavu.
Hata hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, sio watoto wote wanaoishi na ulemavu wanaoweza kujiunga na shule hiyo, kutokana na raslimali finyu shuleni humo.
Hakujakuwa na mpango wowote wa kujengwa kwa shule zingine katika eneo la Pwani zitakazotoa huduma za masomo kwa wanafunzi wanaoishi na ulemavu.
Tangu miaka ya tisaini, idadi ya shule hizo katika eneo la Pwani imesalia pale pale huku shule zinazotambulika zaidi kwa kutoa huduma bora kwa wanafunzi zikikumbwa na uhaba wa vifaa na madarasa.
Wanaoishi na ulemavu hawana la kujivunia licha ya taifa hili kupitia kwa katiba kutoa fursa kwa jamii hiyo kupata nafasi za uwakilishi katika nyadhfa mbali mbali serikalini.
Kulingana na mshirikishi mkuu wa jamii ya walemavu eneo la Pwani Hamisa Zaja, uwakilishi katika nafasi mbali mbali za kitaifa na katika serikali za kaunti bado hazijazingatiwa.
Zaja alisema kuwa wanawake wanaoishi na ulemavu bado wamesalia kutengwa katika uwakilishi.
Alisema kuwa licha ya matumaini ya katiba iliyopitishwa mwaka 2010 kutoa mwongozo uliowapendelea, bado bunge la kitaifa na mabunge ya kaunti hayajapitisha sheria zinazofaidi jamii hiyo.
Alisema kuwa wengi huona kuwa walemavu hawana mchango muhimu katika jamii.
Aidha, amependekeza uteuzi wa nyadhfa mbali mbali serikalini kufanywa kwa kuzingatia kila jimbo huku akiongeza kuwa kwa sasa wanandeleza hamasa kwa jamii ya walemavu ili kujitolea kushiriki katika siasa kwenye uchaguzi mkuu ujao.