Seneta James Orengo katika hafla ya awali. Picha/ nation.co.ke
Seneta wa Kaunti ya Siaya James Orengo amewataka wakaazi wa Mombasa kumpigia kura kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ili aweze kuwa rais ifikapo mwezi Agosti.Orengo alisema kuwa chama cha ODM kitahakikisha Raila anaibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu ujao.“Nina imani kuwa Raila ataibuka mshindi katika uchaguzi ujao, nawaomba mumpigie kura kwa wingi,” alisema Orengo.Aidha, ameikosoa serikali ya Jubilee kwa kujaribu kuwakandamiza viongozi wa upinzani hasa kwa kuwafungulia mashtaka yasiyokuwa na msingi wowote ili wasiweze kugombea nyadhifa za uongozi.Orengo amewataka viongozi wa Jubilee kuheshimu uongozi wa Kaunti ya Mombasa hasa wanapozuru eneo hilo.Orengo alikuwa akizungumza katika Mahakama ya Mombasa muda mchache baada ya Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Mishi Mboko kuondolewa mashtaka ya uchochezi na chuki.