Mwenyekiti wa chama cha ODM eneo bunge la Nakuru Magaribi Shem Osiago ametaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wale wanaotumia vyama vya kisiasa kuleta migawanyiko ya kikabila.
Akizungumza na mwandishi huyu jumanne alasiri, Osiago alisema kuwa siasa kwa misingi ya kikabila imepitwa na wakati, na wale wanaoendesha siasa hizo wanafaa washtakiwe kwa mujibu wa sheria.
Vile vile aliongeza kuwa ingawa katiba inaruhusu vyama vingi vya kisiasa humu nchini, kila mtu ana uhuru wa kujiunga kwa chama chochote, lakini visitumiwe kuleta migogoro na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa hili.
Alisema kuwa ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007, zilizowapelekea zaidi ya wakenya elfu moja mia tano kupoteza maisha yao na wengine wengi kupoteza mali zao, wakenya hawako tayari kurudi katika nyakati hizo.
Ingawa kaunti ya Nakuru ni eneo lenye makabila yote arobaini na mbili, mwenyekiti huyo alisizitiza haja ya utangamano kwa nia ya kuleta amani, umoja na upendo katika kaunti ya Nakuru.
Hata hivyo, Osiago aliwashauri wakazi wa kaunti hiyo na wakenya kwa ujumla kuyapuuza matamshi ya baadhi ya wanasiasa aliyoyataja kuwa hatari na ya kuleta chuki ambao nia yao ni ya kuleta mafarakano katika nchi.
Haya yanajiri huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 ukikaribia.